Friday, 10 July 2015

Tantrade yaunganisha wazalishaji 180 kwa wanunuzi 15


Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mussa UlediMAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imefanikiwa kuunganisha zaidi ya wazalishaji 180 na wanunuzi 15 katika bidhaa mbalimbali ambazo ni korosho, ufuta, mboga na matunda, elimu na machapisho.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mussa Uledi alisema hayo wakati akifunga maonesho ya 39 ya biashara na kusema kuunganishwa huko kumefanyika katika mikutano ya kibiashara kwa washiriki wa maonesho hayo.

Alisema mazungumzo hayo ya kibiashara yafuatiliwe kwa kushirikiana na sekta binafsi ili yazae matunda.
Uledi alisema maonesho ya mwaka huu yamefana kutokana na maandalizi mazuri, bidhaa zenye ubora wa hali ya juu zilizotokana na ubunifu mkubwa kwa wazalishaji, utangazaji wa bidhaa na wataalamu wa masoko wenye kutoa maelezo fasaha kuhusu bidhaa na huduma zao.

Alisema amepata faraja kuwa na mabanda maalumu ya bidhaa za aTanzania kwa ajili ya kutangaza bidhaa za nchini, banda la asalina lile la elimu na kutoa ushauri wa kubainisha bidhaa zingine ili nazo zitafutiwe mabanda maalum ili zionekane na kutangazwa kwa lengo la kutafuta masoko.

Alisema serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili maonesho hayo yaendelee kuwa na kiwango cha kimataifa kwani mafanikio ya maonesho hayo yanahitaji ushirikiano wa serikali na wazalishaji wa bidhaa na watumiaji.
Mkurugenzi wa TANTRADE, Jacqueline Maleko aliwashukuru washiriki wote na kuwakaribisha katika maonesho ya mwakani aliyoahidi kuwa bora zaidi.

No comments:

Post a Comment